
Ikisiri Bwana Yesu asifiwe ni miongoni mwa semo ambazo hutumiwa mara kwa mara na baadhi ya waumini wa makanisa ya Kikristo. Licha ya usemi huo kuwa na maana yake ya msingi, hutumiwa kwa dhima mbalimbali za kipragmatiki. Makala hii inalenga kuchunguza dhima hizo ili kuongeza maarifa kuhusu namna muktadha unavyochangia kupata maana katika lugha. Matokeo kutoka katika sharika tatu za Kanisa la Kilutheri yanaonesha kwamba usemi Bwana Yesu asifiwe una dhima mbalimbali, zikiwamo kusalimia, kuanzisha mazungumzo, kuziba pengo la ukimya, kusisitiza jambo na kuchangamsha waumini. Kwa kuzingatia matokeo haya, makala hii inahitimisha kwamba dhima za usemi Bwana Yesu asifiwe zinaweza kueleweka vizuri pale msikilizaji anapohusisha muktadha wa kiutamaduni, kipragmatiki na kilongo husika.
Ikisiri Taarifa za matamshi katika kamusi zina umuhimu mkubwa katika kuwawezesha watumiaji kutamka maneno kwa usahihi na kuelewa tofauti za kifonolojia zinazojitokeza katika lugha. Mapungufu katika taarifa hizo yanaweza kuathiri uwazi na usahihi wa utamkaji wa maneno, hali inayoweza kuwapotosha watumiaji wa kamusi hizo, kama wanafunzi, walimu na watafiti, na hivyo kupunguza kuaminika kwa kamusi hizo. Makala hii inalenga kutathmini taarifa za matamshi katika Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la Pili (2015) ili kubaini uzingatiaji wa kaida za kifonolojia za Kiswahili sanifu. Uchambuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Fonolojia Zalishi na Nadharia ya Leksikografia. Matokeo yanaonesha kuwa, licha ya jitihada za kuwasilisha baadhi ya vipengele vya matamshi kwa usahihi, bado kuna upungufu katika usilabi, urefu wa irabu, mkazo na matumizi ya alama za unukuzi zisizo sahihi katika baadhi ya vipengele. Makala inapendekeza maboresho ya kitaaluma ili kuimarisha usahihi na uelewekaji wa taarifa hizi. Maboresho hayo ni muhimu kwa ajili ya kuongeza ubora na manufaa ya kamusi kwa watumiaji ikizingatiwa kuwa kamusi hii ni ya taasisi muhimu katika kukuza na kuendeleza Kiswahili Nchini Tanzania.